MBUNGE NGAYIWA AWA MBOGO KWA WATENDAJI WAZEMBE

 

Mbunge wa Jimbo la kahama Mjini Mhe. Ngayiwa Benjamini Lukubha

Mbunge wa Jimbo la kahama Mjini Mhe. Ngayiwa Benjamini Lukubha amewataka watendaji wa Serikali ambao hawapo tayari kufanya kazi za kuwatumikia wananchi ni bora wapishe kwani hayupo tayari kufanya kazi na watendaji ambao wanadhorotesha juhudi za kuwaleta wananchi  wa Jimbo lake Maendeleo.

Mhe. Ngayiwa alisema hayo Aprili 11, 2026 Kahama Mjini kata ya Majengo alipokuwa akihutubia katika Mkutano ulioandaliwa kwa lengo la kuwashukuru wananchi ambao walijitokeza kumchagua katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Alisema hakugombea kufanya maigizo bali aligombea nafasi ya ubunge kwa lengo kwa kuwatumikia wananchi na kusaidiana Pamoja na watendaji Kwenda kushughulikia kero zilizopo katika Mji wa Kahama. 

“ Mliponichagua nikaingia, mimi nilitaka nifanye kazi vizuri na watendaji wetu, kwa sababu nao ni watu wazima wenye akili timamu ambao wengine nui baba na mama wa familia na wengine ni viongozi, hivyo sikuona sababu ya kuanza kufokeana bila sababu niliona sio mzuri.” Alisema 

“ kuna baadhi ya watendaji walianza kusema tumempata Mbunge mpole sasa nataka kuwaambia kwamba upole nauweka pembeni twendeni tukafanye kazi ya wananchi, na wale wote tuliowaalika na nitakaowaalika kwenye mikutano yangu, wasipokuja bila sababu ya msingi maana yake huyo hataki kufanya kazi ya wananchi.” Aliongeza 




Alisema kuwa yeye sio mhandisi wa kujenga Barabara wala sio mtaalamu wa ujenzi wala sio mtaalamu wa kutandaza mabomba wala sio mtaalamu wa kilimo hivyo anapowaalika wataalamu lengo lake wamsaidie sasa wasipotokea maana yake wanataka kumkwamisha katika kuwatumikia wananchi, kwahiyo nikiona mtendaji anataka kunikwamisha sintomvumilia kwa sababu natekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.” Alisema 

Alitolea mfano Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Phantom – Mjini Mkandarasi alitakiwa kumaliza kazi ya ujenzi wa Barabara tangia mwezi wa tisa mwaka 2025 lakini aliongezewa muda bila kukamilisha mradi, hivyo wakakubaliana Pamoja na madiwani wa halmashauri kutoendelea nae wapate mkandarasi mpya ili akamilishe kazi na muda si mrefu watasaini mkataba na Mkandarasi Mpya.




“ siko tayari kuona mambo yakienda tofauti kwani niko hapa kusimamia pesa zinazotolewa na Mhe. Rais Samia  ambazo zimeletwa ili zifanye kazi zilizokusudiwa.” Aliongeza


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama  Thomas  Muyonga


 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama  Thomas  Muyonga aliwataka wananchi wa Kahama kumpa ushirikianao Mbunge wao Ngayiwa kwani ana maono makubwa na Mji wa Kahama na kazi ya kwanza ni kushughulikia Barabara za Kahama.

“ Alipoingia Ngayiwa akishirikiana na meya Pamoja na madiwani wao chama kiliwaagiza kuanza kushughurika na mkandarasi anayechelewesha mradi wa ujenzi wa Barabara ya Phantom -Mjini, na hilo limeshafanyika mpaka sasa tunasubiri Mkandarasi Mpya aanze kazi ya kukamilisha Barabara hii.” Alisema

Aliwaomba wakazi wa Kahama na wakazi wa Majengo kutoa ushirikiano wa Mbunge na madiwani wao  ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika kwa wakati kwani Ngayiwa na wenzake ni wazalendo na wana nia ya dhati kuwatumikia wananchi wa Kahama.


Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani




Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani alimtaka Mhe. Ngayiwa kutokata tamaa na changamoto anazokutana nazo katika kazi yake ya kuwawakilisha wananchi, kikubwa ni kuzidi kumuomba Mungu na kuwataka watu wa Kahama kumpa Ushirikiano. 

“ Ahsanteni kwa kumchagua Ngayiwa kwa kura nyingi, pamoja na Rais Samia na madiwani wote kwani  Mmenipatia kijana mzuri, msikivu, na mtu wa watu niwaombe wananchi wa kahama Benjamini naijua kahama na shida za kahama anazifahamu niwaombe mpeni ushirikiano kwani matatizo ya kahama anayajua, shida ya kahama ni miundombinu mibovu….hivyo Ngayiwa atashughulikia.” Alisema

Katibu wa siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Wa Shinyanga Ndugu Richard Raphael Masele

Naye Katibu wa siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Wa Shinyanga Ndugu Richard Raphael Masele amewapongeza wakazi wa Kahama kwa kumchagua Mhe. Ngayiwa kwanza ni kijana, mchapakazi na mwenye maono.

“ Nina hakika Kahama mmepata Mbunge wa kuwaletea maendeleo wala hamjakosea, na mtegemee kupata maendeleo yatakayomwagika Kahama. Mbunge huyu amechaguliwa kushughulikia kero na changamoto za Barabara na kwa kuanza wameanza na mkandarasi aliyekuwa nachelewesha mradi na tayari ameshaondolewa atakuja mwingine na mradi utakamilika.” Aliongeza


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Ndugu Mabala Mlolwa







Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Ndugu Mabala Mlolwa ambaye alikuwa  Mgeni Rasmi katika Mkutano huo aliwashukuru wananchi wa Kahama kwa kumchagua Rais Samia, Mbunge Ngayiwa na Madiwani wote wa Jimbo la Kahama Mjini kwa kura nyingi.

Akimzungumzia Mhe. Ngayiwa alisema jambo kubwa lililomsukuma kugombea nafasi hiyo ni uchungu wa wana Kahama kwa ubovu wa mindombinu ya Barabara ikiwemo kutokamilika kwa wakati hivyo akalazimika kuchukua fomu agombee  ili aondoe hizo kero.

“ Hakuja kwenye ubunge kufanya maigizo angeendelea kukaa benki na kupata mshahara aliumia nani Mtanzania anayeipenda Kahama alienda mpaka kwa Rais mguu kwa mguu alimfata na mimi ni shaidi akamwambia Mhe. Rais Barabara tuliizungumzia huyu Kandarasi ameibomoa mpaka sasa hivi watu wangu wanakula vumbi….. Ngayiwa akasema huyu Kandarasi hatufai, Madiwani walianzisha ila Ngayiwa amefanikisha kuondolewa kwa Mkandarasi.” Alisema





Katika Mkutano huo Mhe. Ngayiwa alipokea kero mbalimbali za wananchi na watendaji wa halmshaauri walizipokea na zilizotakiwa kutolewa ufafanuzi zilijibiwa. 









Mkutano huo ulihudhuriwa na Madiwani  wa Kahama Mjini, Mstahiki Meya na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi Mkaoni Shinyanga na Wilaya ya Kahama. 





































 








 


0/Post a Comment/Comments