Na Atley Kuni, WAF- Tabora
Serikali
imezindua rasmi mafunzo muhimu ya wataalam wa afya yanayolenga
kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na uchakataji sahihi wa takwimu za
maabara nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za afya
na mifumo ya taarifa za kitabibu.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mafunzo hayo Aprili 13, 2026 mkoani Tabora, Kaimu
Msajili wa Baraza la Wataalam wa Maabara nchini Bi Zubeda Salumu amesema
mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu iliyotekelezwa mwaka 2025 kwenye
Hospitali za Mikoa, ambapo wataalam wa maabara walipatiwa ujuzi wa
ufuatiliaji wa magonjwa na uteuzi wa waratibu wa (Laboratory based
surveillance) wanaoendelea kuripoti taarifa za wiki kwa mafanikio
makubwa.
Amesema kutokana
na mafanikio hayo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI na
Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mradi wa Pandemic Fund imeamua
kupanua wigo wa mafunzo hadi ngazi ya msingi ili kuwafikia watumishi
wengi zaidi wa sekta ya afya nchini.
“Lengo
kuu ni kuhakikisha watumishi wa afya wanapata uelewa wa kutosha kuhusu
ufuatiliaji wa magonjwa pamoja na uchakataji sahihi wa takwimu za
maabara, kwani ngazi ya msingi ndio mwanzo wa mambo mengi” amesema Bi.
Zubeda.
Aidha, amesema
Maabara ni kitovu muhimu cha takwimu za afya, hivyo ni muhimu kwa
wataalam wa maabara kuwa na ujuzi wa kuzichakata na kuzitumia ipasavyo
kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.
Kwa
upande wake Kaimu Msajili Bodi ya Maabara binafsi nchini (PHLB), Bw.
Emmanuel Mjema yeye amewataka washiriki hao, kuchukulia jukwaa hilo la
mafunzo kama kitu pekee cha kuwaimarisha katika utendaji wa kazi zao za
kila siku.
Mara baada ya
kukamilika kwa mafunzo hayo washiriki watapatiwa alama za maendeleo
endelevu ya kitaaluma (CPD), ambapo taratibu za upatikanaji wake
zitaelezwa na waratibu wa mafunzo.
Kwa
upande wake mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Afya amewataka
washiriki hao kuhakikisha wanalipia leseni zao za kitaaluma ili
kuondokana na usumbufu wakati wautekelezaji wa majukumu yao kwenye
vituo.


.jpg)



Chapisha Maoni