Macho
na masikio ya Watanzania sasa yameelekezwa Aprili 3, 2026, tarehe
ambayo inatazamwa kama kilele cha safari ya kutafuta ukweli na uponyaji
wa kitaifa baada ya matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotikisa wakati na
baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Tume
ya Uchunguzi wa Matukio hayo, inayofanya kazi chini ya Sheria ya Tume
za Uchunguzi (Sura ya 32), inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ambayo
wataalamu wa saikolojia wanaamini itakuwa zaidi ya karatasi za kisheria,
bali ni kiponyo cha majeraha ya kihisia yaliyowaacha wengi na makovu ya
chuki na hofu.
Baada
ya kuongezewa siku 42 tangu Februari, tume hiyo sasa imefika ukingoni
mwa mchakato uliolenga kuchimba mizizi ya machafuko hayo na kutoa
mapendekezo yatakayorejesha hali ya utulivu kisaikolojia kwa wananchi
walioathirika.
Mtaalamu
wa saikolojia, Jesusa Malewo, anabainisha kuwa ripoti hii inatarajiwa
kuwa mwarobaini wa kupunguza hasira na chuki zilizokuwa zimeanza kuota
mizizi ndani ya jamii kutokana na migawanyiko ya kisiasa.
Kwa
kueleza sababu za kweli za machafuko hayo, ripoti itasaidia kufuta
tetesi na propaganda ambazo mara nyingi huwa ni mafuta kwenye moto wa
migogoro. Malewo anaamini kuwa hatua hii itasaidia serikali kubaini
udhaifu wa kimfumo, hasa katika nyanja za usalama na michakato ya
uchaguzi, huku ikitoa fursa kwa taifa kujifunza kutokana na makosa yake
ili kuzuia jinamizi kama hilo lisijirudie katika chaguzi zijazo.
Kwa
upande mwingine, mdau wa masuala ya kijamii, Richard Chiligati, anaona
ripoti hiyo kama darasa tosha kwa wanasiasa ambao ndio wahusika wakuu
katika ujenzi wa demokrasia.
Anasititiza
kuwa matokeo ya uchunguzi huo yatatoa muongozo wa kipi cha kufanya na
kipi cha kuepuka ili kudumisha mshikamano wa kitaifa, huku akiwakumbusha
viongozi umuhimu wa kuwasikiliza wananchi wao.
Ni
matarajio ya wengi kuwa kila kitakachowasilishwa na tume kitaleta imani
mpya kwa wanasiasa na wadau wa demokrasia, kikithibitisha kuwa amani si
tu kukosekana kwa vita, bali ni uwepo wa haki na utawala wa sheria
unaoeleweka na kila mmoja.
Uwasilishaji
wa ripoti hii Aprili 3 hautakuwa tu mwisho wa kazi ya tume, bali mwanzo
wa safari mpya ya kuimarisha ustahimilivu wa taifa letu katika
kukabiliana na migogoro bila kuingia kwenye taharuki.
Jamii
inasubiri kuona mapendekezo yatakayoboresha sera na mifumo ya utawala,
ikiamini kuwa ukweli utakaowekwa wazi utakuwa msingi wa kuunganisha tena
vipande vya amani vilivyovunjika. Huu ni wakati wa kusubiri matokeo kwa
matumaini, tukiamini kuwa dawa itakayotolewa na tume hiyo itakuwa na
nguvu ya kuunganisha mioyo ya Watanzania na kuijenga upya Tanzania yenye
mshikamano wa dhati.
Chapisha Maoni