
Shirika
la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania) kwa kushirikiana na
Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola
na Maendeleo (FCDO), wametoa zaidi ya Shilingi milioni 70 kama mtaji wa
awali kwa biashara bunifu zilizoanzishwa na wanafunzi wa vyuo vikuu
nchini.
Msaada
huo umetolewa katika msimu wa pili wa Mpango wa Kubadilishana Ujuzi
miongoni mwa wahadhiri wa vyuo vikuu Afrika Mashariki, uliofanyika kwa
siku tatu katika Chuo cha Indian Institute of Technology Madras (IIT
Madras) kampasi ya Zanzibar.
Mpango
huo uliwakutanisha wanafunzi wabunifu, viongozi wa vyuo vikuu,
wakufunzi na wadau wa mfumo wa ubunifu kwa lengo la kuimarisha nafasi ya
vyuo vikuu kama chachu ya ujasiriamali na ubunifu.
Programu
hiyo inaendeleza mafanikio ya toleo la kwanza lililojulikana kama RISE
4.0, ambalo limekuwa likiwasaidia wabunifu vijana kubadilisha mawazo yao
kutoka vyuoni na kuyageuza kuwa biashara halisi zinazoweza kukua.
Mpango huo unatekelezwa na UNDP kupitia Mradi wa FUNGUO kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza kupitia FCDO. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuwaunganisha wanafunzi na ushauri elekezi, fursa za ufadhili pamoja na mazingira yatakayosaidia mawazo yao kukua na kuwa biashara endelevu.
Mpango huo unatekelezwa na UNDP kupitia Mradi wa FUNGUO kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza kupitia FCDO. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuwaunganisha wanafunzi na ushauri elekezi, fursa za ufadhili pamoja na mazingira yatakayosaidia mawazo yao kukua na kuwa biashara endelevu.
Kabla
ya kutangazwa kwa washindi, timu za wanafunzi zilipata mafunzo na
ushauri kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu shiriki pamoja na wadau wa
mfumo wa ubunifu.
Mafunzo
hayo yalihusu uundaji wa mawazo ya biashara, kukuza biashara changa,
mikakati ya kuingiza ubunifu sokoni na namna ya kujenga biashara
zinazoweza kupanuka na kushindana sokoni.
Jumla
ya biashara bunifu sita ziliingia fainali za mwaka huu ambazo ni
Vestis, Naarad, CropIQ, Carbon Trace, Ecofy na Power Taka.
Mshindi
wa jumla, Vestis, biashara iliyoanzishwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, ilipokea Shilingi milioni 15 kama mtaji wa awali. Jukwaa
hilo la kidijitali linalenga kurahisisha ununuzi na uuzaji wa nguo
mtandaoni na kuwasaidia watumiaji kuokoa muda na gharama za usafiri.
Mbali
na mtaji huo wa awali, biashara hizo bunifu pia zitapata msaada
endelevu ikiwemo fursa za kuwasilisha mawazo yao kwa wawekezaji, mafunzo
ya masoko na uendeshaji wa biashara, ushauri elekezi pamoja na fursa za
kujenga mitandao na wadau wa ubunifu na wawekezaji watarajiwa.
Akizungumza
katika hafla ya utoaji tuzo, Meneja wa Mpango wa FUNGUO wa UNDP
Tanzania, Joseph Manirakiza, alisema toleo la pili la mpango huo
linaonyesha dhamira ya UNDP katika kukuza ubunifu kwa vijana nchini.
Alisema
kupitia mpango huo, zaidi ya biashara bunifu 70 zinazoongozwa na
wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali tayari zimenufaika.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji
wa Teknolojia (COSTECH), Dkt. Erasto Mlyuka, alisema serikali inaunga
mkono programu zinazochochea ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi wa
vyuo vikuu.
Alisema
vyuo vikuu vinapaswa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa ujasiriamali ili
wanapohitimu wawe tayari kuanzisha biashara zao badala ya kutegemea
ajira pekee.
Akizungumza kwa niaba ya timu iliyoshinda, mwakilishi wa kampuni ya Vestis, Kelvin Erasto, alisema fedha hizo zitasaidia kupanua jukwaa la biashara hiyo na kuwafikia watumiaji wengi zaidi.
Alisema
pia wanatarajia kuendelea kupata mafunzo na ushauri kutoka kwa
wataalamu wa vyuo vikuu ili kuimarisha mtindo wao wa biashara na
kuharakisha ukuaji wake.
Mpango
huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Vyuo Vikuu kama Injini za
Ubunifu: Kujenga Njia Endelevu kutoka Maarifa mpaka Biashara.”
Katika
mkutano huo wa siku tatu uliofanyika kuanzia Machi 4 hadi 6, wahadhiri
wa vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa ubunifu walijadili namna taasisi
za elimu ya juu zinavyoweza kuchochea zaidi uanzishaji wa biashara
bunifu, uendelezaji wa tafiti zenye tija kibiashara na ukuaji wa
biashara zinazoendeshwa kwa ubunifu nchini Tanzania na Afrika Mashariki.
Kupitia ujenzi wa uwezo, ushauri elekezi na mtaji wa awali, mpango huo unalenga kuimarisha biashara bunifu zinazozaliwa vyuoni ambazo zina uwezo wa kuzalisha ajira, kutatua changamoto za maendeleo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa ubunifu nchini.











Chapisha Maoni