WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba
amesema kuwa Serikali inatambua uwepo wa watumishi wa umma
wanaochapakazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu
huku wakijiepusha kujiingiza katika makundi ya wazembe, wezi na
wanaofanya kazi kwa mazoea.
“Serikali haitomuonea mtu, watumishi
wachapakazi wasiingie ubaridi kwa sababu Serikali inatambua mchango wao
katika maendeleo ya Taifa. Watu wasome alama za nyakati Serikali
haitovumilia masuala ya wizi kwa sababu yanarudisha nyuma maendeleo.”
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Machi 09, 2026 wakati akizungumza
na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Namanyere
wilayani Nkasi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. Miongoni mwa
malengo ya ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa
Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kufanya
kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya udokozi kwa sababu
havikubaliki na havivumiliki, hivyo wahakikishe wanatekeleza majukumu
yao ikiwemo kusimamia ipasavyo ujenzi wa miradi.
Pia, Waziri Mkuu
amesisitiza mikoa yote kuhakikisha katika upangaji wa bajeti wanaweka
vipaumbele vya uchimbaji wa visima kupitia mitambo iliyosambazwa katika
mikoa yao. “Mitambo ya uchimbaji maji itumike kuchimba visima ili
wananchi wapate maji ya uhakika.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amezitaka mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu au
sheria itakayowabana wakandarasi kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi wao
stahiki zao kwa wakati.
Ametoa agizo hilo kutokana na kumekuwapo
kwa malalamiko ya baadhi ya wakandarasi kutowalipa wafanyakazi
wanaofanya kazi katika miradi ya ujenzi hata pale wanapokuwa
wameshalipwa na Serikali kwa kazi walizotekeleza.
Mheshimiwa Dkt.
Mwigulu ametoa agizo hilo baada ya wananchi waliofanykazi katika miradi
mbalimbali kueleza kero ya kutolipwa na wakandarasi licha ya
wakandarasi hao kuwa tayari wamelipwa na Serikali.
Kwa upande
wao, wabunge wa mkoa wa Rukwa wameipongeza Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao ikiwemo
ya afya, elimu na kilimo.
Miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa
Nkasi Kaskazini Salum Kazukamwe ambaye alishukuru kwa ujenzi wa hospital
ya wilaya ambayo inakwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za
afya, ambapo pia, mbunge huyonameiomba Serikali kumalizia ujenzi wa
kituo cha afya cha Kebwe.




Chapisha Maoni