
Balozi wa Serbia nchini, Mhe. Jovica Topalović, amesema, maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, yanaipa Tanzania fursa ya kuimarisha mazingira ya shughuli za kidiplomasia na uhusiano na mataifa mbalimbali.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa Serbia, ambapo alipongeza hatua za Serikali katika kuendeleza eneo hilo. Amesema anaamini ndani ya miaka 10 ijayo, balozi nyingi zitahamia Mtumba, jambo litakaloimarisha nafasi ya Dodoma kuwa kama kitovu cha shughuli za kidiplomasia nchini.
Aidha, amesema uwepo wa balozi nyingi katika eneo moja utarahisisha mwingiliano na ushirikiano wa kidiplomasia. Pia ameongeza kuwa, Serbia na Tanzania zina historia ndefu ya uhusiano na maeneo mbalimbali ya ushirikiano na akieleza matumaini ya kuimarika zaidi kwa uhusiano huo katika miaka minne ijayo.
Katika
ziara hiyo, Mratibu wa Ujenzi na Uendelezaji wa Mji wa Serikali, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Bw. Noel Mlindwa, aliwasilisha taarifa kuhusu maendeleo
ya ujenzi na uendelezaji wa eneo hilo. Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani kutoka Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu, pamoja na
Maafisa wa Wizara na wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Chapisha Maoni