Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura,
akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati
ya MCT na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika mkoani Morogoro
Julai 16–17, 2026. Mkutano huo unajadili mafanikio, changamoto na
mustakabali wa tasnia ya habari nchini katika kipindi cha miaka 30 ya
mfumo wa kujisimamia.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, akifungua
Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya MCT na viongozi wa vyombo
vya habari unaofanyika mkoani Morogoro Julai 16–17, 2026.
Katibu
Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura (katikati), akiwa katika picha ya
pamoja na washiriki wa Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya MCT
na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika Morogoro Julai 16–17, 2026.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Baraza
la Habari Tanzania (MCT) limeendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda
uhuru wa vyombo vya habari, kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari na
kusimamia maadili ya wanahabari nchini kwa kipindi cha miaka 30, huku
likitoa mchango mkubwa katika kujenga tasnia yenye uwajibikaji na
kuaminika nchini.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest
Sungura, wakati akifungua Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano kati ya
MCT na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika Morogoro Julai 16–17,
2026, ambapo amewasilisha tafakuri ya miaka 30 ya mfumo wa kujisimamia
kwa sekta ya habari nchini.
Amesema
katika kipindi hicho MCT imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha
tasnia ya habari, huku pia ikitathmini changamoto zinazoikabili sekta
hiyo na kupendekeza hatua za kujenga mustakabali imara wa uandishi wa
habari nchini Tanzania.
“Kwa
miaka 30 MCT imeokoa vyombo vya habari kwa usuluhishi nje ya mahakama,
imejengea uwezo waandishi wa habari, imefanya uchechemuzi wa sera na
sheria mbalimbali zinazohusu tasnia, imeandaa na kusimamia kanuni za
maadili ya uandishi wa habari zinazotumika kitaifa na mfumo wa
kujisimamia umetambuliwa kimataifa kama mfano wa usimamizi wa
kitaaluma,” amesema Sungura.
Hata
hivyo, Sungura amebainisha kuwa mafanikio hayo yameambatana na
changamoto zinazoendelea kuikabili MCT na sekta ya habari kwa ujumla.
Ametaja
mshikamano wa sekta umedhoofika, uchumi wa vyombo vya habari umedorora
na sekta bado inakabiliwa na changamoto za uhuru wa vyombo vya habari,
kupungua kwa imani ya umma kwa vyombo vya habari na kuongezeka kwa hofu
kuhusu usalama wa wanahabari.
Akizungumzia
mustakabali wa sekta hiyo, Sungura amependekeza kuanzishwa kwa mfuko
endelevu wa kusaidia vyombo vya habari kiuchumi na kufanyika kwa
marekebisho ya sera na sheria ili maamuzi ya MCT yatambuliwe kisheria.
Aidha,
amezitaka taasisi za habari kubuni vyanzo vipya vya mapato kupitia
huduma za kidijitali, usajili wa wanachama, matukio maalumu, matangazo
na huduma za data, huku akisisitiza umuhimu wa kurejesha imani ya umma
kupitia maadili, uwajibikaji na weledi.
Mkutano
huo umeandaliwa na MCT kwa kushirikiana na VIKES –ambayo ni taasisi ya
Finland ya Vyombo vya Habari na Maendeleo, ukiwakutanisha viongozi 21 wa
sekta ya habari, wakiwemo wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari na
mameneja wa vyumba vya habari.
Washiriki wanajadili changamoto zinazoibuka na fursa mpya zinazoathiri mustakabali wa uandishi wa habari nchini.
Mkutano
huu unafanyika wakati sekta ya habari ikikabiliwa na kasi ya mabadiliko
ya teknolojia za kidijitali, matumizi yanayoongezeka ya akili unde
(AI), mabadiliko ya matarajio ya jamii, changamoto za usalama wa
wanahabari na hitaji la kuimarisha ubora wa taarifa pamoja na kurejesha
imani ya umma kwa vyombo vya habari.
































































Chapisha Maoni