Mkuu
wa zamani wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Ernest Mangu, ametoa wito
kwa Watanzania kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake
kuendeleza mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa amani ni rasilimali
muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Akizungumza
katika mahojiano maalum yaliyochapishwa na gazeti la Uhuru, Mangu
alisema kuwa ishara zozote za kuchochea vurugu au kuvuruga utulivu wa
nchi zinapaswa kukemewa mapema, akionya kuwa gharama za kupoteza amani
ni kubwa na huathiri sekta zote za uchumi na ustawi wa jamii.
“Tuna
wajibu wa kulinda amani yetu. Historia inaonyesha kuwa pale amani
inapovunjika, athari zake huwa pana, zikigusa uchumi, uwekezaji na
maisha ya watu kwa ujumla,” alisema.
Mangu
alieleza kuwa Tanzania imejijengea sifa ya kuwa nchi yenye utulivu kwa
muda mrefu, hali ambayo imeiwezesha kuvutia uwekezaji na kukuza shughuli
za kijamii na kiuchumi. Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanapaswa
kulindwa na kuendelezwa kupitia uwajibikaji wa wananchi na taasisi zote.
Kwa
mujibu wake, baadhi ya mienendo inayoibuka katika jamii, ikiwemo
matumizi mabaya ya majukwaa ya mawasiliano na kauli za uchochezi,
inaweza kuhatarisha mshikamano uliopo kama haitadhibitiwa kwa wakati.
“Amani
si jambo la kubahatisha. Inahitaji nidhamu, utii wa sheria na
ushirikiano wa wananchi wote. Pale ambapo kuna dalili za kuvurugika kwa
utulivu, hatua zichukuliwe haraka kuzuia madhara makubwa,” aliongeza.
Aidha,
alisisitiza umuhimu wa vyombo vya dola kufanya kazi kwa weledi na haki,
akibainisha kuwa utekelezaji sahihi wa sheria ni nguzo muhimu ya
kulinda utulivu wa nchi. Alisema wananchi wanapaswa kuwa na imani na
taasisi za usalama na kushirikiana nazo katika kudumisha amani.

Chapisha Maoni