Mratibu wa kituo cha lishe cha Ufundiko kilichopo wilayani Kongwa Bwana Rashid Mtalumba amesema kuwa zaidi ya miaka kumi iliyopita kituo chao kiliweza kuhudumia watoto 30 wenye utapiamlo lakini mpaka sasa kutokana na lishe bora na elimu wanayotoa wamefanikiwa kupunguza idadi ya watoto wenye utapiamlo hadi kufikia watoto wanne kufikia Januari 2025.
Akiongea
na waandishi wa habari Mtalumba amesema kituo cha lishe cha Ufundiko
kinajihusika na utoaji wa lishe bure kwa watoto wenye umri wa miaka
mitano wenye utapiamlo na kutoa maziwa (Lactogen 1)kwa watoto wachanga
ambao mama zao hufariki baada ya kujifungua, wapo katika Kata 9 na
vijiji 25 ndani ya Wilaya ya Kongwa vikiwemo vijiji vya Norini matongoro
na mautya.
Aidha amesema
Ufundiko wanashirikiana na Serikali katika masuala ya lishe na kutoa
msaada kwa watoto wenye utapiamlo uliopitiliza kwa kuwapeleka katika
hospitali mbalimbali nchini Tanzania kama vile Benjamin Mkapa, Muhimbili
na Mlali kwenye kituo cha mazoezi kwa watoto wenye ulemavu.
Ameeleza
kuwa watoto wengi wenye utapiamlo ni wale wanaozaliwa na watoto yaani
wasichana wadogo wenye umri chini ya miaka 18 wengi wao baada ya
kujifungua huondoka na kukimbilia mijini kufanya kazi za ndani na
kuwatelekeza watoto na bibi zao ambapo hujikita na shughuli za shamba
badala ya kutunza watoto.
Mtalumba
amesema changamoto kubwa inayojitokeza katika suala la lishe kwa
watoto ni kuwa wanaume au kina baba wengi hawashiriki katika kupata
elimu ya lishe pindi inapowafikia vijijini kwa kuendekeza mfuko dume wa
kuwa mwanamke ndiye mwenye jukumu la kupeleka watoto kliniki na sio
mwanaume.
Mtalumba
ameeleza wasiwasi wake kutokana na Mabadiliko ya hali ya hewa kuwa
yanaweza kuathiri sana suala la lishe kutokana na uhaba wa mvua kwani
hata chakula cha kawaida kinaweza kisipatikane kwa wananchi.
Bw
Mtalumba ameshauri Serikali kupitia kwa maafisa ugani kuendelea kutoa
elimu kwa wananchi waweze kulima mazao yanayostahimili ukame kama mtama
au watumie njia ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa
chakula aidha wazazi watoe chakula kwa kuzingatia makundi ya chakula kwa
kutumia vyakula vya asili.
Akiongea
katika mkutano wa wadau wa Lishe uliofanyika katika ukumbi wa hospitali
ya Wilaya ya Kongwa mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe Mayeka Simon Mayeka
amewapongeza wadau hao wa lishe wakiwemo ufundiko na Cuamn kwa mchango
mkubwa wanaoutoa katika kusaidia Serikali katika masuala ya lishe na
kupunguza idadi ya watoto wenye utapiamlo.
Aidha
Mayeka amesisitiza wananchi kutunza mazingira na kuendelea kutunza
chakula walichonacho kwani hali ya hewa iliyopo sio nzuri mvua ni ndogo
kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababishwa na uharibifu wa
mazingira uliofanywa na bianadamu.
Source: KongwaDc



Chapisha Maoni